UINGEREZA MAREKANI WAMPA TANO UHURU KENYATA
Nairobi, Kenya. Muda mfupi baada ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake
William Ruto kuapishwa jana, Marekani na Uingereza zilituma salamu za
pongezi na zikaahidi kushirikiana na Kenya huku zikitoa wito wa
kufanyika majadiliano kuondoa migawanyiko katika jamii.
Salamu za pongezi kutoka kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May
ziliwasilishwa na Waziri wa Masuala ya Afrika Rory Stewart aliyehudhuria
sherehe za kuapishwa kwa Rais Kenyatta na naibu wake na akasema tukio
hilo la Jumanne ni fursa kwa Kenya kusonga mbele baada ya uchaguzi
uliochukua muda mrefu.
Taarifa kutoka ofisi inayoshughulikia masuala ya Jumuiya ya Madola
imesema Rais Kenyatta anakaribishwa kwenye mkutano wa Jumuiya hiyo
utakaofanyika London mwakani.
“Huu ni wakati ambao Kenya inaweza kusonga mbele baada ya uchaguzi
uliorefushwa, kusababisha migawanyiko na kuingia na ari mpya ya
maridhiano,” alisema Stewart.
“Natumai kwamba Wakenya wote watatambua haja sasa ya kuingia kwenye mjadala wa kitaifa na kuponya makovu.”
Katika hatua nyingine, taarifa ya maandishi ya Marekani imesema
inatarajia kuimarisha ushirikiano na kurejesha ushirikiano baina ya nchi
mbili hizo katika miaka michache ijayo.
Serikali ya Marekani imeelezea wasiwasi wake kuhusu mgogoro wa kisiasa
unaoendelea nchini na matumizi makubwa ya nguvu yasiyo ya lazima dhidi
ya raia na imetoa wito wa kufanyika mjadala wa kitaifa kama sehemu ya
mchakato wa kukabili mgogoro huo.
"Tunawahimiza Wakenya kuungana na kufanya majadiliano ya wazi, endelevu
nay a haraka kwa ajili ya kuponya migawanyiko katika jamii,” imesema
taarifa ya Marekani.

Maoni
Chapisha Maoni